KWA mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mgogoro wa umeya jijini
Arusha, mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema (CHADEMA), jana alishiriki
kikao cha Baraza la Madiwani ambacho kiliongozwa na mwenyekiti wa muda,
Diwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe (CHADEMA).
Mgogoro wa umeya jijini Arusha, ulichukua sura mpya baada ya madiwani
wa CCM kuwazunguka wenzao wa CHADEMA mwaka 2010 na kumchagua Gaudence
Lyimo kuwa meya, jambo lililozua tafrani kubwa.
Baadaye mgogoro huo ulikua, huku CHADEMA wakiendelea kutomtambua meya
huyo, jambo ambalo lilisababisha madiwani wao watano kuvuliwa
uanachama baada ya kufikia muafaka hewa na CCM.
Katika uchaguzi mdogo wa kata hizo nne Julai mwaka huu, CHADEMA
iliibuka kidedea na hivyo kuzua hofu kuwa huenda ikatumia wingi wake
kumng’oa meya, hatua ambayo Lema alisema si ajenda yao kwa sasa bali
kuwatumikia wananchi.
Jana wakati baraza hilo lilipokutana, Diwani wa Kata ya Sokon 1,
Michael Kivuyo (TLP), alikieleza kikao kuwa Meya Lyimo amesafiri,
hivyo amemkaimisha ofisi kutokana na halmashauri hiyo kutokuwa na naibu
meya.
Taarifa hiyo iliibua mjadala huku madiwani wakitaka kanuni zifuatwe,
ndipo Diwani wa Kata ya Levelos, Ephata Nanyaro (CHADEMA),
alimpendekeza Msofe awe mwenyekiti wa muda wa kikao hicho.
Katika kura zilizopigwa, Msofe alipata 13 za kumkubali huku nne zikimkataa.
Kikao hicho kiliibua hoja ya upotevu wa zaidi ya sh milioni 14.8
ambapo kati yake fedha taslimu ni zaidi ya sh milioni 8.6 zilizodaiwa
kwisha kutokana na makato ya benki ya kuhudumia akaunti.
Matumizi mengine ni vifaa kwa ajili ya ujenzi wa tarafa ikiwemo
saruji na mchanga vyenye thamani ya zaidi ya sh milioni 6.3 ambavyo
vilichangwa na wananchi.
Madiwani hao walimuagiza kaimu mkurugenzi wa jiji, Afwilile Lamsy,
kuhakikisha kwenye kikao kijacho analeta taarifa za kibenki za akaunti
iliyowekwa fedha hizo mwaka 2004 ili kuona namna zilivyokatwa hadi
zikaisha.
“Tunataka kuonyeshwa taarifa za benki tujue namna fedha hizo
zilivyotumika, hatutaki kuona barua za mawasiliano ya mkurugrnzi na
mkuu wa wilaya, tunataka wale wote waliohusika waletwe hapa hata kama
walihamishwa watafutwe waletwe.
“Hii ni fedheha kubwa, haiwezekani wananchi wachange fedha halafu
zipotee hivi hivi tu, tunataka tuletewe hapa taarifa za benki na
tupelekwe tukaone mchanga na saruji vilivyonunuliwa,” alisema Diwani wa
Kata ya Ngarenaro, Doita Isaya (CHADEMA).
Pia madiwani hao waliwaagiza wataalamu kupima maeneo muhimu ikiwemo
mito, hifadhi za barabara na maeneo ya milima na kuyawekea alama ili
kuyalinda yasivamiwe kama hali inavyoonekana kwenye maeneo mengi ya
jiji la Arusha.
|
No comments:
Post a Comment