HOTUBA
YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KATIKA UFUNGUZI WA TAMASHA LA MATUMAINI, UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM, TAREHE
07 JULAI, 2013
Ndugu
Wananchi;
Nakupongeza sana ndugu Erick Shigongo kwa
kuandaa tamasha hili adhimu lenye mchanganyiko wa mambo mengi. Bahati nzuri
mambo yote ni mazuri na yanayalifanyia taifa letu mambo mema. Sala ya pamoja
kuliombea taifa, burudani mbalimbali zikiwemo za muziki, mchezo wa ngumi na
mpira wa miguu.
Pengine faida kubwa zaidi ya Tamasha lenyewe
hili ni kujenga moyo wa upendo, umoja, ushirikiano na moyo wa uzalendo miongoni
mwa Watanzania wa marika yote: watoto, watu wazima na wazee. Miongoni mwa watu
wa makabila yote, rangi zote, dini zote na miongoni mwa wafuasi wa vyama vyote
vya siasa.
Katika
kipindi hiki ambacho maadui wa umoja, amani na utulivu wa nchi yetu wanahangaika
usiku na mchana kuleta mifarakano miongoni mwa Watanzania, matukio kama Tamsha
hili ndilo jibu zuri kwao. Kupitia Tamasha kama hili tunawajibu kuwa Watanzania
hatutaki, hatukubali na wala hatudanganyiki. Tuwapelekee ujumbe huo bila
kumung’unya maneno kuwa njama zao zimeshindwa na kamwe
hazitafanikiwa.
Lakini,
tamasha hili pia lipeleke ujumbe kwa wanasiasa na wafuasi wao kuwa kutafuta
umaarufu, kuungwa mkono au ushindi kwa kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania
kwa misingi ya dini zao, rangi zao, na maeneo watokayo nako hakutawasaidia.
Walishindwa wakoloni kwa sera yao ya wagawe uwatawale, hataweza mswahili.
Isitoshe ni kutenda dhambi kubwa na kutowatendea haki Watanzania, Mungu wao,
dini zao na vyama vyao vya siasa kuingiza dini katika siasa au siasa katika
dini. Kiongozi wa siasa anayesema dini yetu ni hii au kiongozi wa dini anayesema
Chama chetu ni hiki wote ni wababaishaji. Wanasema mambo ambayo hayana uhusiano
wo wote na dini. Kiongozi wa dini huyo awe mkweli tu kwamba, ni mwanachama au
mpenzi wa Chama cha siasa aliyeamua kutumia nafasi yake ya uongozi wa dini au
uumini wake kuendeleza maslahi ya Chama chake. Hakuna lolote la dini hapo na
wala hakuna kitabu kitakatifu cha dini yoyote kinachotaja Chama cha siasa cha
kufuata.
Kiongozi wa siasa anayetumia dini kujenga Chama
chake amefilisika hoja za kisiasa. Isitoshe Sheria ya Usajili wa Vyama iko wazi.
Inazuia kutumia udini, ukabila na aina zote za ubaguzi. Watu hawa wamegubikwa na
tamaa ya madaraka iliyovuka mipaka ya utu. Sijui kama watu hawa hawatambui
athari zake. Tunaweza kufika siku makanisa na misikiti ikagawanyika kwa upenzi
na ufuasi wa vyama vya siasa. Tutazikwaza dini zetu na nchi yetu kuiweka mahala
pabaya.
Tuwaache wanasiasa na wanachama wagawanyike kwa
vyama vyao wanavyovipenda lakini makanisa na misikiti pawe mahali pa
kuwaunganisha. Mwenyezi Mungu awe ni muunganishaji wao. Lakini tukiendelea na
mikakati ninayoiona na kuisikia inaendelea hata katika nyumba za ibada, viongozi
wa dini watashindwa kuwaunganisha waumini wao. Badala ya watu kutambuana kama
Waislaimu au Wakristo wataanza kujuana kwa vyama vya siasa. Ni hatari kubwa kwa
dini kwani upenzi wa watu kwa vyama vya siasa ni vitu vinavyobadilika kulingana
na sera, matukio na mazingira. Hivi tunataka na imani ya watu kwa dini iwe
inabadilika na mazingira?
Tuyalinde mambo yanayotuunganisha ili yadumu.
Tusiyaendekeze mambo yanayotugawa. Pale ambapo siasa zinagawanisha, dini,
michezo na mengineyo yanayowaunganisha yatekelezwe kwani yanaweza kusaidia
kupunguza uhasama na yanaweza kusaidia kuponya. Zitto Kabwe na William Ngeleja
wako vyama viwili vinavyoshindana katika majukwaa ya siasa, lakini leo watacheza
upande mmoja wa Wabunge wa Simba. Halima Mdee, Grace Kiwelu, Mohamed Misinga wao
ni viongozi wa Yanga Bungeni. Mambo yanayotuunganisha tuyape kipaumbele
kusisitiza umoja wetu, kujenga upendo na kupunguza makali ya tofauti
zetu.
Ndugu
Shigongo wa Global Publishers nakupongeza sana kwa kufanya jambo linaloponya
jamii. Matukio kama haya yanatakiwa yawe mengi zaidi nchini kwani yana manufaa
makubwa kwa nchi yetu na watu wake. Sisi katika Serikali tunaunga mkono.
Yaendelezeni na yadumisheni.
Nakushukuru pia kwa uamuzi wako wa busara wa
kutumia asilimia 20 ya pesa zinazokusanywa kusaidia ujenzi wa mabweni ya
wasichana katika shule nane za sekondari katika mikoa ya Manyara, Tanga, Dodoma,
Lindi, Ruvuma, Mara, Mwanza na Kigoma. Ni jambo jema sana. Asante
sana.
Kwa
ndugu zangu Wabunge, wasanii wa muziki na filamu na wanamichezo wengine
waliojitolea kutuburudisha leo nawapongeza na kuwatakia kila heri. Tumekuja
kuwashuhudia na kuburudika nanyi. Naomba mtuburudishe na kuwaonyesha vijana kuwa
ujuzi hauzeeki.
Kwa
mara nyingine nashukuru kualikwa.
Asanteni
sana.
No comments:
Post a Comment