Iwapo Urusi imeamua kuchukua jukumu la kuleta pande mbili zinazozana katika vita vya Syria katika meza ya mazungumzo ya amani ni kwasababu ya dalili kuwa Marekani huenda ikajipata polepole katikati ya mzozo huo
Tangazo la pamoja kati ya Urusi na Marekani mapema wiki hii kuwa zitajaribu kuwaleta pamoja wawakilishi wa utawala wa Rais Bashar al Assad na waasi wanaotaka kumngoa madarakani Assad inaashiria mpango wa kwanza muhimu wa kidiplomasia katika kipindi cha karibu mwaka mmoja.
Baada ya mazungumzo ya kina mjini Moscow siku ya jumanne, Marekani na Urusi zilisema zitajaribu kupiga jeki makubaliano ambayo nchi hizo mbili ziliidhinisha mwezi Juni mwaka jana,makubaliano ambayo yaliacha wazi swali la iwapo Assad anapaswa kuachilia madaraka au la.
Wazo la nchi hizo mbili ni kushawishi pande zote mbili katika mzozo wa Syria kusogea katika meza ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanywa mjini Geneva mwishoni mwa mwezi huu ili kujaribu kumaliza vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe na kuundwa kwa serikali ya mpito kwa maafikiano ya pamoja.
Mchakato huo wa kumaliza vita ambavyo vimesababisha vifo vya watu 70,000 tangu vianze mwaka 2011 ulibuniwa kwa kile sasa kinachojulikana kama Mawasiliano ya Geneva Juni 30,2012.
Mabadiliko ya misimamo kuhusu Syria
Baada ya Urusi kutoonyesha ari ya kutaka mpango huo kutekelezwa mwanzoni, kubadilika kwa mtazamo huo sasa na kuonyesha nia ya kutaka kufufua wazo hilo la upatanishi huenda ikaashiria kuwa Rais wa Marekani Barrack Obama anatafakari upya msimamo wake wa kupinga kutumia njia za kijeshi katika mzozo huo wa Syria.
Dalili za mkengeuko wa mawazo ni pamoja na kukiri kwa Ikulu ya Marekani tarehe 25 mwezi uliopita kuwa asasi za kijasusi za nchi hiyo zinaamini kuwa serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake,jambo ambalo Obama hapo awali alitaja kama kigezo cha kuashiria kuvuka mipaka.
Kuna ishara pia kuwa mzozo huo unasambaa,Israel ilifanya mashambulio yaliyolenga maeneo kadhaa nchini Syria mwishoni mwa juma lililopita na hofu ya kuwepo kwa wanamgambo wa kiislamu wenye itikadi kali katika vita hivyo wengine walio waaminifu kwa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda na vile vile mchango wa Iran na washirika wake Hezbolla wa Lebanon wanaomuunga mkono Assad.
Kwa upande mwingine kuna sauti kubwa ya wamarekani wanaomshurutisha Rais Obama kuwapa silaha waasi. Miongoni mwa wanaomshurutisha ni Seneta Robert Menendez mwenyekiti wa kamati ya senate yenye ushawishi mkubwa ya masuala ya mambo ya kigeni ambaye alianzisha mswada kuhusiana na kupewa silaha kwa waasi wa Syria tarehe 6 mwezi huu.
Obama bado yuasita kuhusu majeshi yake Syria
Obama amedhihirisha wazi kuwa hana nia ya kutumia jeshi lake katika vita vya Syria huku akiwa amewarejesha wanajeshi wa taifa lake kutoka vita vya Iraq na anajaribu pia kukamilisha jukumu la wanajeshi wake walio katika vita vya Afghanistan.
Wanadiplomasia wanasema iwapo hili litabadilika,kuwapa silaha waasi itaonakana kama hatua ya mwanzo badala ya mashambulio ya moja kwa moja dhidi ya Syria kama mashambulio ya angani na kutuma majeshi ya Marekani nchini humo.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov baada ya mazungumzo na mwenzake wa Marekani John Kerry siku ya Jumanne alisema Urusi haizingatii tu hatma ya baadaye ya Rais Assad ila wanajali hatma ya raia wa Syria.
Hata hivyo wachambuzi wanatilia shaka uwajibikaji wa Urusi kwa hilo la kusitisha mahusiano ya karibu na Rais Assad kwani wanadai hakuna mabadiliko ya kupigiwa mfano katika uhusiano wa washirika hao wawili katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters
Mhariri: Amina Abubakar.
Mhariri: Amina Abubakar.
No comments:
Post a Comment