KIKUNDI cha waasi wanaopigana vita ya msituni dhidi ya majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, kimerudia kuwaonya wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walioondoka hivi karibuni kwenda kujiunga na vikosi vya kulinda amani nchini humo, kuwa wasijiingize katika vita na waasi hao, limeandika gazeti la Mtanzania
Kimesema iwapo wanajeshi wa Tanzania watathubutu kuwashambulia waasi hao, nao watalipiza kisasi kwa kujibu mapigo.
Onyo hilo limetolewa mapema wiki hii na rais wa kikundi hicho, Bertrand Bisiimwa(Pichani juu), katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili, yaliyofanyika kwa njia ya simu kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika mahojiano hayo, Bisiimwa alitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali aliyoulizwa na MTANZANIA Jumapili, huku akisisitiza kuwa vikosi vya wapiganaji wake vina rekodi nzuri ya kuvishinda vikosi vya majeshi ya kigeni, hata kama vina silaha za kisasa.
Alionya kuwa wanajeshi ya Tanzania wanaoelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kulinda amani, wanapaswa kufanya hivyo na si vinginevyo, kwa sababu iwapo watavishambulia vikosi vyake, havitasita kuingia vitani kukabiliana na wapiganaji wa JWTZ.
Bisiimwa alisisitiza kuwa wanajeshi wa Tanzania wanapaswa kuzingatia onyo hilo ili kuepusha umwagikaji wa damu ya majirani zao wa kihistoria ambao ni raia wa Kongo.
Akizungumzia ubora wa vikosi vya wapiganaji wake, alisema ni wa hali ya juu, kwa sababu vinaundwa na wanajeshi waliowahi kulitumikia Jeshi la Serikali ya Kidemokrasia ya Kongo, hivyo linao askari wenye uzoefu wa kutosha katika medani za vita.
MTANZANIA Jumapili lilipomdadisi kuhusu uwezo wa zana za kivita walizonazo wapiganaji wake na idadi yao, Bisiimwa alikataa kuzungumzia hayo, lakini aliendelea kusititiza kuwa wapiganaji wake wapo imara kukabiliana na shambulizi lolote dhidi yao na kwamba wanazo zana za kivita za kisasa na za kutosha.
Alipoulizwa iwapo barua aliyomuandikia Rais Jakaya Kikwete na ile aliyoielekeza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa na lengo la kutoa vitisho au ililenga kueleza msimamo wa kuwa tayari kupigana vita na wanajeshi wa Tanzania, alisema haikuwa na lengo la kulitisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, bali kulionya na kulikumbusha kuzingatia kwenda kulinda amani pekee badala ya kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya M23.
Katika hatua nyingine, rais huyo wa waasi alikanusha tuhuma zinazoelekezwa kwa kikundi chake kuwa kinapatiwa msaada wa silaha za kivita kutoka baadhi ya mataifa ya ukanda wa maziwa makuu, kwa kuelekeza kuwa silaha za kisasa wanazomiliki zilichukuliwa kutoka kwenye jeshi la Serikali ya Kongo.
“Nasema hapana, habari hizi za silaha tumekuwanazo sisi kwa masiku mingi…ujuwe baada ya kuondokana na jeshi la Serikali ya Kinshasa, tulichukuaga masilaha mingi ambayo tumekuwa nayo siku zote, hivyo siyo kweli kwamba kuna ‘any country’ inasapoti sisi kuhusu masilaha,” alisema Bisiimwa.
Biisimwa pia alikanusha vikosi vyake kutumia wapiganaji watoto, kwa kile alichoeleza yeye na wenzake kama raia Kongo na M23 anapigania maisha ya wakongomani, anatambua suala la kulinda watoto ni jukumu lao la kwanza katika eneo lililo chini ya himaya ya vikosi vyake.
Alisema vikosi vya wapiganaji wake vinashikilia eneo kubwa la Mashariki ya Kongo na kuitaja miji ya Kivu Kaskazini na Goma yenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi kuwa ngome yao kuu.
Alilitaka gazeti hili kuifahamisha dunia kuwa kikundi cha M23 kinaundwa na raia wa Kongo wanaopambana na majeshi ya serikali dhidi ya maslahi ya Wakongomani wote wanaoonewa na utawala wa Rais Joseph Kabila.
Aliishutuma Serikali ya Rais Kabila kwa kudai inawaonea na kuwatesa Wakongomani wanaoishi eneo la Mashariki ya nchi hiyo, jambo lililowasukuma kuwapigania.
“Mabaya kuhusu M23 ni mapropaganda za bawatu, kweli bakongomani wa eneo hili la Mashariki wamekuwa chini ya maisha ya uonevu na kunyanyaswa kwa makumi ya miaka mingi, dhamana yetu kama M23 ni kuwalinda bandugu zangu dhidi ya waharifu wanaotumwa na Serikali ya Kinshasa.
“Ukiufahamu ukweli kuhusu maisha ya binadamu huku, hakika utatupilia mbali mapropaganda ya kutukandamiza sisi…unajua huku kuna misitu minene, sasa ikifika saa 10 jioni inabidi mtu asitoke nje ya nyumba, la sivyo akiendelea kuwa nje anaweza kuuawa au kubakwa na maharamia ambao wanapewa sapoti na Serikali ya Kinshasa kwa makusudi ya kuichonganisha M23 na Jumuia za Kimataifa,” alisema Bisiimwa.
Alidai kuwa Serikali ya Kinshasa inakiuka misingi na malengo ya kusimamia umoja wa Wakongomani kwa kuendekeza demokrasia za chuki na uonevu.
“M23 inapigania uhuru wa bakongomani, hivyo sisi sote ni raia wa Kongo, tunaipenda nchi yetu na migogoro inayoendelea ndani ya nchi yetu tutaimaliza wenyewe, nichokitaka kwa Serikali ya Kinshasa itekeleze mkataba wetu wa makubaliano ya amani wa mwaka 2009.
“Kama Serikali ikikubali kurudi nyuma na kushirikiana nasi kuridhia mkataba huo hakuna tatizo la amani hapa nyumbani, lakini sioni umuhimu wa kuhitaji majeshi kutoka nje pasipo kukaa nasi katika meza moja ya kutatua mgogoro huu, sisi sote ni Wakongo na tunahitaji kuiletea maendeleo nchi yetu,” alisema Bisiimwa.
MTANZANIA Jumapili lilimuuliza Bisiimwa iwapo wapiganaji wake ndio waliohusika na shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi mkoani Arusha, ambapo alieleza kuwa hakuna mpiganaji wake hata mmoja aliyehusika kupanga au kutekeleza uhalifu huo.
Alisema wapiganaji wa M23 hawajahusika na mlipuko huo na aliwaonya maadui wa himaya yake kutolitumia tukio hilo dhidi ya wapiganaji wake.
“Natoa pole kwa bandugu zagu batanzania kutokana na tukio hilo la kinyama ambalo limesababisha vifo vya watu batatu na bengine makumi sita kupata majeraha, M23 imeguswa sana. Tanzania ni bandugu zetu wa enzi na enzi, sisi Bakongomani tunaiheshimu historia ya umoja wetu na Tanzania hivyo siasa ya Mwalimu Nyerere siku zote imekuwa mwanga na ‘direction’ ya maisha yetu sote,” alisema Bisiimwa.
Kauli hii ya Bisiimwa imekuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Kimataifa, Bernard Membe, kulitangazia taifa kuwa Serikali ya Tanzania haiogopa vitisho vilivyotolewa na waasi wa M23, ambao waliandika barua kwa Rais Kikwete wakionya hatua ya kupeleka jeshi nchini Kongo kuwa inaweza kusababisha vita.
Waziri Membe alisema ameiona barua ya waasi hao ambayo pia ilielekezwa kwake na Ofisi za Bunge, ikiwa la lengo la kutoa vitisho kwani waasi hao wanaviogopa vikosi vya wanajeshi wa Tanzania.
“Kuhusu M23 nimepata barua wizarani na bungeni imeletwa, hiyo barua wanasema imeandikwa kwangu na Mungu na kuwa imesainiwa na Mungu, hawa wanatutisha kama tulivyotishwa na Kanali Mohamed Bakari alipokuwa ameiteka Anjouan, pamoja na vitisho vyote alivyotoa, yeye ndiye aliyeishia kutoroka akiwa amevaa baibui.
“M23 wanaua, wamebaka, wamedhalilisha wazee na mama, wameleta wimbi la wakimbizi zaidi ya 220,000, halafu wanamnukuu Mwalimu Nyerere wakisema binadamu wote ni sawa, huko ni kukufuru, kama wangekuwa wanathamini kauli ya Mwalimu wangeliua? Wangebaka? wangedhalilisha wazee?” alisema Membe.
Alisema serikali ya Tanzania itapeleka vikosi vya wapiganaji wake Kongo na vitatakiwa kutekeleza mambo matatu aliyoyataja kuwa ni kuhakikisha wapiganaji wa M23 hawajipanui kutoka idadi ya wapiganaji 600 wa sasa, kudhoofisha kundi hilo kwa kuondoa silaha mikononi mwao na kujenga uhusiano.
No comments:
Post a Comment