Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akionyesha alama ya ‘V’ wakati akitoka Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya rufaa dhidi yake kutupiliwa mbali. Wa pili kulia ni Wakili wake, Tundu Lissu. Picha na Michael Jamson
Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema
ameibuka kidedea baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya
marejeo ya rufaa iliyomrejesha bungeni.
Maombi
hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na makada watatu wa CCM mkoani
Arusha, kupitia kwa Mawakili wao Alute Mughway na Modest Akida
wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kwa
madai kuwa hukumu hiyo haikuwa sahihi.
Hata
hivyo, jana Mahakama ya Rufani ilisikiliza maombi hayo kutoka kwa
waombaji pamoja na hoja za wajibu maombi na kisha kutupilia mbali
maombi hayo ikisema kuwa hayana msingi.
Uamuzi
huo wa kutupilia mbali maombi hayo ulisomwa na Jaji Bernard Luanda, kwa
niaba ya jopo la majaji wenzake lililokuwa likiongozwa na Engela Kileo
na Salum Massati.
Hata hivyo, jopo hilo halikutoa sababu za kutupilia mbali maombi hayo na badala yake lilisema litatoa maelezo ya kina baadaye.
Majaji
hao isipokuwa Kileo ndiyo waliosikiliza na kutoa hukumu ya rufaa
iliyomrejesha Lema bungeni, ambayo ilikuwa inapingwa na makada hao wa
CCM.
Awali,
kabla ya kutupilia maombi hayo ya marejeo, mahakama hiyo ilitupilia
mbali maombi ya waombaji hao kutaka suala hilo lisikilizwe na jopo la
majaji saba.
Wakili
Mughwai aliwasilisha maombi katika Mahakama ya Rufani akiomba marejeo
ya rufaa yahamishwe katika jopo la majaji watatu na kupelekwa
kusikilizwa na jopo la majaji saba kwa madai kuwa kuna jambo linatakiwa
kushughulikiwa kutokana na mazingira yake.
Wakili
wa Lema, Methods Kimomogoro alidai kuwa Wakili Mughwai amechanganya
maombi hivyo kuleta utata na kwamba kama alikuwa akitaka yasikilizwe
angeyapeleka katika utaratibu ulio sahihi.
No comments:
Post a Comment