TAARIFA KWA UMMA
MAUAJI YA MWANACHUO WA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA (HENRY KAGO) NA KAULI YA CHAFU YA MKUU WA MKOA WA ARUSHA
Ndugu wanahabari na wakazi wote wa mkoa wa Arusha.Kwanza kabisa, tunapenda kutoa pole za dhati kwa familia, ndugu jamaa, wanachuo na jumuia yote ya chuo cha uhasibu Arusha wa marehemu Henry Kago aliyefariki juzi usiku kwenye tukio la kutisha na kuhuzunisha sana.
Tumesikitishwa na msiba huu na tunawaombea wote Mungu awapatie faraja na utulivu katika kipindi hiki kigumu.
Katika tukio hili, mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema alijulishwa na kama kiongozi alifika ili kuona namna atakavyoweza kutoa msaada hasa baada ya wanachuo kuonyesha hisia zao kwa vile hawakuona kupata msaada kutoka kwa uongozi wa chuo na serikali kwa ujumla. Hili ni tukio la pili la mauaji ya mwanachuo sambamba na matukio mengi ya wanachuo kuvamiwa na kunyang’anywa mali zao.
Mhe Lema aliwatuliza wanachuo na kuchukua hatua za kumjulisha mkuu wa Mkoa Mhe Mulongo aje na kuzungumza na vijana hawa.
Hata hivyo ujio wa mhe Mulongo ulionekana haukuwa na dhamira ya dhati na badala yake alionyesha madharau makubwa ambayo mpaka sasa nashindwa kuelewa alikuwa na maana gani kuonyesha tabia ya kipuuzi namna ile kwa vijana waliokuwa wamepata msiba wa mwenzao.
Picha za video zinaonyesha kwa dhahiri jitihada kubwa aliyoifanya mhe Lema kuwatuliza vijana hawa na kuwaomba wawe wavumilivu.
Baada ya tukio zima kukumbwa na vurugu ambazo kimsingi chanzo ni tabia aliyoinyesha Mhe mulongo kwa vijana hawa, mkuu wa mkoa aliongea na waandishi wa habari kuwa chanzo cha vurugu hizo ni Mhe Lema na kuwa tukio zima la mauaji haya ni masuala ya kisiasa na kuwa wanasiasa wamepanga mambo haya ili kujipatia umaarufu, hii na kauli ya mwendawazimu kabisa.
Katika hatua hii walimkamata Wakili Mhe Albert Msando ambaye pia ni diwani wa CHADEMA na kumchukua kwa mahojiano.
Kwa ujumla msingi wa suala la kumtafuta muuaji wa Henry umepabadilika na kuwa kumtafuta Lema.
Tunataka tuweke kumbukumbu hii kwa wakazi wa Arusha, jambo hili ni mfululizo wa matukio mengi yasiyoonyesha weledi ya Mhe mulongo ambayo amekuwa akifanya na kama chama tunamtakia hivi kikombe kitakopajaa atatambua maana ya nguvu ya umma.
Anaweza kudharau maneno haya, afanye hivyo kwa vile anajisikia kuwa yupo na mamlaka ya kiserikali lakini tunarudia kusema kuwa kamwe hatuwezi kuendelea kuvumilia uongo na akili mbovu za namna hii kuongoza watu wenye akili. Narudia kusema hatutavumilia uongo wa namna hii kuendelea kusemwa halafu familia iliyopoteza mtoto wao mpendwa ikiwa katika masononeko makubwa.
Sasa mhe Mulongo na watu wake wajiandae vema maana tumejiandaa kupambana na watu na/au viongozi ambao tumeshajua ni wapotoshaji na wahuni na wanafanya mambo ya kihuni.
Tunawaomba wakazi wa Arusha wawakatae viongozi wapotoshaji na wahuni, wasiwape ushirikiano wowote ule na sisi tutasimama na wananchi kwa pamoja katika mazingira yote ili kudumisha uongozi bora wenye kujali na kuheshimu raia wote kwa mustakabali wa mkoa wetu kiuchumi na katika kujenga utulivu.
Imetolewa leo tarehe 25 Aprili 2013
Amani Golugwa
KATIBU WA CHADEMA – KANDA YA KASKAZINI.
No comments:
Post a Comment