Pages

March 24, 2013

WAANDISHI WAPEWE MAFUNZO YA KUJIHAMI

WAANDISHI WAPEWE MAFUNZO YA KUJIHAMI
Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kupata mafunzo ya jinsi ya kujihami kufuatia baadhi ya waandishi kufanyiwa vitendo vya utekaji na uteswaji.
Mafunzo hayo ya kujihami yameelezwa kuwa ni muhimu hasa kwa waandishi wanaofanya habari za uchunguzi ambao licha ya kufanya kazi ya kufichua ukweli ili kuisaidia jamii wamekuwa katika mazingira hatarishi ya kutishiwa na kushambuliwa pindi wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kujilinda wao na vitendea kazi vyao.
"Wote mnafahamu kuwa wako watu wanaotapanya mali za umma na pia wako viongozi wanaotumia vibaya madaraka yao kwa maslahi binafsi mwandishi anayeamua kufanya uchunguzi juu ya mambo kama haya na kuyagusa  anajikuta anaingia katika hatari kubwa ya kupata vitisho,kushambuliwa ama kupoteza maisha" Alisema Angelo Mwoleka ,Mkurugenzi wa Jambo Printers wanaochapisha gazeti la Kutoka Arusha.
Amesema kuwa ni vyema mafunzo hayo yakaandaliwa na vyama vya waandishi vya mikoani maarufu kama (press club),kuomba mafunzo katika jeshi la kujenga taifa ambalo kwa sasa limefungua milango kwa watumishi wa serikali na wananchi kujiunga na vile vile mafunzo  hayo yatolewe katika vyuo vya habari ili wahitimu waweze kukabiliana na changamoto hiyo pindi wanapokuwa kazini.
Akizungumza katika mahafali ya sita 6 ya Chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Arusha (AJTC) kilichopo eneo la Morombo jijini Arusha, amewataka wahitimu kuepuka kuandika habari za kuwafurahisha watu na kuwapamba kwani wakati huo hauko tena badala yake wajikite kwenye kuandika habari zitakazoisaidia jamii.
Mwoleka amepongeza juhudi za Uongozi wa chuo hicho kwa kuanzisha kikundi cha Tae Kwondo ambacho licha ya mazoezi ya kumfanya mtu awe na afya nzuri pia yanamsaidia kujihami na kuwa ulinzi binafsi wa mtu dhidi ya maadui anaokutana nao na kuvitaka vyuo vingine viige mfano huo .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo wa AJTC,Joseph Mayagila akizungumzia hali ya soko la ajira  amesema kuwa tatizo la ukosefu wa ajira ni la kidunia  hutokana na mabadiliko ya kiteknolojia,kiuchumi na kimazingira  na hilo halimaanishi kuwa ubunifu umekwisha kwani wamekuwa wakitoa mafunzo ya ujasiriamali  na wanafunzi amekuwa wakihimizwa kufanya shughuli za kujiingizia kipato wakati wakiwa chuoni .

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...