Filbert Rweyemamu
Meya wa Jiji la Arusha,Maximillian Iranqhe amesema hatavumilia kuendelea kuona Jiji la Arusha katika mazingira ya uchafu na kumwelekeza Mkuu wa Idara Usafi na Mazingira,James Lebikoki kuwasimimia watendaji walio chini yake kutekeleza majukumu yao ipasavyo wakiwemo wazabuni waliopewa kandarasi za kusafisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha.
Ametoa kauli hiyo leo Januari 4,2026 kwenye Soko la Mbauda lililopo Kata ya Sombetini katika mwendelezo wa kampeni ya “Ng’arisha Jiji ” yenye lengo la kuufanya mji wa Arusha kuendelea kuwa na hadhi ya kimataifa na kuvutia watalii wengi zaidi kwa kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Iranqhe amesema usafi ni tabia inayopaswa kuendelezwa kwasababu uchafu unaweza kusababisha milipuko ya magonjwa na haivutii wanunuzi wenye tabia ya kupenda mazingira yaliyo safi na salama kwaajili yao na wafanyabiashara.
“Natoa wito kwa Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira simamia kikamilifu watu walio chini yako,ninakujua vizuri wewe ni mchapakazi mzuri lakini wasaidizi wako wanakuangusha usipowachukulia hatua haraka nitakuchukulia hatua na wakandarasi ambao hawatimizi wajibu wao tunaweza kuvunja mikataba yao,”amesema Meya Iranqhe
Amesema wakati anashika nafasi ya Umeya miaka mitano iliyopita Jiji la Arusha lilikua nyuma kiusafi lakini kwa kushirikiana na viongozi wenzake wamefanikiwa kuufanya mji kuwa safi lakini kuna dalili za ulegevu zinazoweza kurudisha nyuma juhudi hizo na kuahidi kuwachukulia hatua wazembe wote bila kumwonea aibu mtumishi au mzabuni yeyote.
“Wafanyabiashara ni muhimu mfanye shughuli zenu katika mazingira yaliyo safi na salama hata wateja wanapokuja wawakute mpo sehemu safi,nakuagiza Katibu wa Soko la Mbauda hakikisha kabla na baada ya shughuli zenu mnaacha mazingira ya biashara zenu yakiwa safi,”amesema Iranqhe
Diwani ya Kata ya Sombetini,Gedfrey Kitomari amesema iwapo wananchi watashirikishwa kusimamia usafi kwenye mazingira yao wapo tayari kuitikia wito wa serikali kwani umuhimu wa mazingira yaliyo safi unawahusu wananchi wote wakiwemo wafanyabiashara.
“Soko la Mbauda ni muhimu kwa uchumi wa wakazi wa Kata ya Sombetini na jiji la Arusha kwa ujumla,ushuru unaopatikana unasaidia kuboresha miundombinu na shughuli nyingine za maendeleo kampeni hii ya Ng’arisha Jiji itakua endelevu kwa wananchi wetu,”amesema Kitomari
Kwa upande wake,Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Jiji la Arusha,James Lobikoki ameahidi kutekeleza maagizo ya Meya kwakua yapo kwenye mpango wa kuhakikisha Jiji la Arusha linalozalisha zaidi ya tani ngumu za taka Tani 360 kila siku linakua safi.
Meya wa Jiji la Arusha,Maxmillian Iranqhe (wa pili kulia)akizungumza wakati zoezi la kufanya usafi Soko la Mbauda Kata ya Sombetini jiji la Arusha.
Wananchi wakifanya usafi eneo la Soko la Mbauda.





Post a Comment