Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka akimkabidhi fedha Bw. Methesela
Mrobi wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa
Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba,
Wilaya ya Busega Mkoani humo.
Na Stella Kalinga
Mkuu
wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka viongozi wa kata na vijiji
kuwabaini wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya TASAF III (PSSN)
wanaojihusisha na ulevi na kuwaondoa katika orodha ya wanufaika wa
mpango huo.
Mtaka
ametoa agizo hilo wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha
Mwamgoba wilayani Busega katika zoezi la uhawilishaji fedha za TASAF III
PSSN, ambapo jumla ya shilingi 2,976,000 zimegawiwa kwa wanufaika 82
kijijini hapo.
Mtaka
amesema lengo la mpango wa TASAF III ni kuwatoa watanzania katika hali
ya umaskini kwa kuwapa ruzuku itakayowasadia kupata huduma muhimu ikiwa
ni pamoja huduma za afya, kuwasaidia watoto wao waweze kwenda shule
lakini baadhi ya wanufaika wamekuwa wakitumia fedha hizo kulewa badala
ya kuanzisha miradi midogo midogo kama ufugaji wa kuku, mbuzi na kondoo
pamoja na kilimo ili miradi hiyo iwasaidie kuwaongezea kipato.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka akizungumza na wakazi wa Kijiji
cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo pichani) kabla ya zoezi la
uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya
maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
“Hatuwezi
kuleta fedha tukifikiri zitawasaidia kujikwamua katika Umaskini lakini
mnashinda baa na vilabuni kulewa , wengine mnaongeza wake, tukiwabaini
mtaondolewa kwenye huu mpango” , alisema Mtaka.
Mtaka
amewataka wanufaika hao kujishugulisha na kilimo na ufugaji na
kuondokana na dhana ya kuwa watakuwa wanufaika wa mpango huo siku zote,
ambapo alieleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwatoa wananchi
katika umaskini na kuwaondolea changamoto mbalimbali kama kutoa elimu ya
bila malipo na kuanzisha Mfuko wa Huduma ya Afya Watanzania wasio na
uwezo waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu na akatoa wito kwa
wanufaika hao kujiunga na Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii (CHF)ambao
utawasaidia wao wenyewe pamoja na wategemezi wao kupata huduma za Afya
katika Vituo vya kutolea huduma za Afya.
Aidha,
ametoa wito kwa wazazi kuwakumbusha watoto wao wajibu wa kuwatunza kwa
sababu kumekuwa na baadhi ya wazee ambao wametambuliwa kuwa ni maskini,
wakati wana watoto wenye nguvu na uwezo wa kuwasaidia lakini hawatimizi
wajibu wao kuwatunza kwa kuwapa mahitaji muhimu.![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEircDNNRpnKEiiqM4dN2hOIjktrEJVvb0poBClPo-ZhsgOGaIqHWuia4JMeJk1bl67a8r1jqSVW6gPIxMWdU8Ezy1Oy9C8FkGaE0U3i9S2-gkscBi-t_D5o23Xr6NMqjf7h9DFl0ictzjNS/s640/PICHA+3.JPG)
Katibu
Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akifafanua jambo kwa wakazi
wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo pichani) kabla ya zoezi
la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya
maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
Akizungumza
baada ya kukabidhiwa fedha hizo Bibi. Christina Robert ambaye ni
mnufaika wa mpango wa TASAF amesema mpango huo umemsaidia kuondokana na
kuishi katika nyumba ya nyasi na matope na kumuwezesha kujenga nyumba ya
matofali na bati.
“Naishukuru TASAF maana imenisaidia sana, ruzuku niliyopewa mara ya
kwanza ilinisaidia kutibiwa nilipofanyiwa upasuaji, mara ya pili
nilitumia tena kwenye matibabu, mara ya tatu nilinunua kuku na bata,
mara ya nne nikanunua bati nikajenga nyumba ya vyumba viwili”, alisema
Christina.
Pamoja
na kusisitiza juu ya matumizi sahihi ya fedha za ruzuku za TASAF Mtaka
amewataka wananchi wa Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuongeza
juhudi katika kilimo cha mazao ya mikunde kwa kuwa tayari Serikali ya
India imekubali kununua zaidi ya tani milioni sita ya choroko, dengu na
mbaazi kutoka Tanzania, hivyo wakati utekelezaji wa makubaliano hayo
utakapoanza wananchi walime kwa wingi mazao hayo kwa kuwa kutakuwa na
soko la uhakika.
Jumla
ya kaya 4260 zilibainishwa katika vijiji 41 vya wilaya ya Busega ambapo
kaya 53 ziliondolewa katika mpango wa TASAF III PSSN baada ya uhakiki na
kubaini kuwa hazikukidhi vigezo.
Baadhi
ya wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III katika kijiji
cha Mwamgoba Wilayani Busega, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani), alipozungumza nao kabla ya zoezi la
uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa ajili ya mpango huo.
Bw.
Methesela Mrobi akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na viongozi wengine
wa Mkoa na Wilaya(hawapo pichani) Bwawa dogo alilochimba kwa kutumia
fedha za ruzuku za Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, ambalo
analitumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji
Mkuu
wa Wilaya ya Busega , Mhe. Tano Mwera (katikati) na Katibu Tawala Wilaya
ya Busega, Bw. Sebastian Masanja (kulia) wakizungumza jambo kabla ya
zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa
kunusuru kaya maskini TASAF III kijiji cha Mwamgoba, Wilayani Busega
(kushoto) Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.(Picha na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu).
No comments:
Post a Comment